Mgombea wa urais wa Marekani wa chama cha Republican, Donald Trump, siku ya Jumatatu alimtakia afya njema mpinzani wake wa chama cha Demokratik, Hillary Clinton, baada ya waziri huyo wa mambo ya nje wa zamani kuugua ugonjwa wa homa ya mapafu, Pneumonia.
Trump aliliambia shirika la habari la Fox News kwamba anatumai kuwa Clinton atapata nafuu haraka na kuweza kushiriki kwenye mdahalo ujao. Mfanyabiashara huyo tajiri aidha amesema kuwa atatoa rekodi zake za hospitali baada ya vipimo alivyofanyiwa hivi karibuni.
Clinton aliahirisha mikutano ya kampeni ya leo Jumatatu na kesho Jumanne katika jimbo la magharibi mwa Marekani la California baada ya kuugua.
Msemaji wa Clinton alisema jana usiku kuwa waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje hatafanya ziara hiyo, ambayo ilitarajiwa kuwa ya kukusanya pesa na kutoa hotuba kuhusu uchumi. Kampeni ya Clinton ilisema kuwa daktari alimpima siku ya Ijumaa kufuatia kikohozi cha muda mrefu, na wakati huo akafahamishwa kwamba alikuwa na homa ya mapafu.
Madaktari walimpa dawaza antibiotics na kumshauri apate mapumziko na kubadilisha ratiba yake. Hata hivyo, maradhi hayo hayakutangazwa hadharani hadi jana Jumapili, pale alipoonekana akiwa mchofu wakati wa maadhimisho ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mjini New York. Clinton aliondoka ghafla na video ilimuonyesha akisaidiwa na watu kabla ya kujikwaa na kuingia kwenye gari.
0 comments:
Post a Comment